Sawaaxili (Baravenes) - "Labada Waddo".mp3 / "السواحيلية - "الطريقان(Baravenes).mp3 //
YOHANE 1
Neno akawa mwanadamu
1Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. 2Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. 3Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. 4Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. 5Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
6Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, 7ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. 8Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. 9Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
10Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. 11Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. 12Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, 13ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe.
14Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
15Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’”
16Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. 17Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. 18Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.